RIWAYA YA ‘IPO SIKU’

Anwani: Ipo Siku

Mwandishi: Solomon Muya

Mapitio: Vera Omwocha

Bei: Shilingi mia tano tu (KSH 500)

Kurasa: 131

Kuagiza: 0720-084-765; 0751-562-750

Kitabu hiki kimechapishwa na Writers Guild Kenya

Riwaya hii inamwangazia kijana mmoja ambaye pia ni msimulizi; Jabali. Akiwa na miaka 12, anapambana na kifo cha mama yake mzazi na kutengwa na dadake aliye na upungufu wa kimaumbile. Babake naye anasafiri kwenda jijini ili kutafuta, wanawe wasimwone kwa miaka mingi.

Jabali na kakake Bahati wanafunga safari ili kuishi na nyanya yao katika kijiji tofauti. Pale kwa nyanya wanapata kwenda shule ila ni Bahati tu aliye mwepesi wa kuelewa na anayezingatia yanayofunzwa shuleni na kutia bidii. Jabali naye anajikakamua kwa kumuiga kakake ila kuwa kwenye orodha ya wanaoshikilia mkia shuleni na kuchekwa na wanafunzi wengine kunamuudhi.

Siku moja, wanafunzi wengine wanapomtania Jabali kwa madharau, msichana mmoja tajiri, Teri anamtetea. Tangu siku hiyo, Jabali anajaribu kumpoza Teri asifanikiwe. Bahati naye anaendelea na masomo hadi anapoitwa kwenye chuo kikuu cha Garissa. Shambulizi la ugaidi linapotokea, swali kuu ni ‘je, Bahati yu hai?’

READ ALSO:  THE STARS CAN WAIT

Wakati mmoja, jua laonekana kuwaka maishani mwake Jabali anapojiunga na familia ya Bwana Muchiri mjini Kakamega. Nyanyake anapougua, anaamua kurudi nyumbani ili kumhudumia. Baada ya miaka michache, rafikiye Jabali anamwalika mjini. Mjini, Jabali anafanya vibarua mbalimbali kujikimu hadi siku moja ambayo Maria, mwanawe Muchiri, anapojitokeza chumbani kwake na kisha kuuawa. Jabali anazingiziwa mauaji na kufungwa miaka kumi.

Jabali anasimulia, “Nilisafiri mpaka mbinguni na kumdadisi Muumba iwapo ipo siku angeumbua machungu ya maisha yangu. Siku nitakapoamka nilikute jua likichomoza, niteremee ndani ya miale ya utanashati wake hadi liende chini nikiwa bado mwenye bashasha. Na giza liingiapo? Nisipatwe kabisa na mitego yake shetani bali nuru ya nyota na mwezi ziniongoze hadi siku za halafu.”

Hadithi hii inaangazia kifo, umaskini, msamaha, uhalifu, mausiano ya kifamilia na kimapenzi, matuamaini ya binadamu na  mengine mengi. Kwa lugha nyepesi, mwandishi anamkaribisha msomaji kufikiria hali ya kibinadamu na kumpa matumaini kuwa kweli yapo machungu maishani lakini ipo siku yatakapotokomea.

“Asiyeifahamu dunia na aitembee polepole. Ni mti mkavu usiotegemewa.”

“Ama kweli, hakuna ajuaye lifanyikalo zaidi ya mwisho wa maisha. Iwapo mfu huzaliwa tena na kuanza maisha upya, iwapo kifo ndicho mwisho wa yote, au labda ipo dunia nyingine ambayo roho ya binadamu inaendelea kuishi.

 

“….Hakuna ndoto zinazopita masilahi ya kuachana na tamaa ya kibinafsi ili kuchunga wengine. Hiyo ndiyo ndoto halisi.”

Jabali, usilolijua ni kuwa kila mtu ni mfungwa katika ulimwengu huu. Haikosi kila anayeishi anang’ang’ania kujitoa minyororo ya jela alizojifunga au kufungwa. Jela zenyewe zaweza kuwa; maradhi, ndoa, mizozo ya kifamilia, umaskini, uongozi wa kimabavu, madawa ya kulevya, chuki, kutamauka, kisasi na mengine mengi…Safari ya maisha ni ukombozi.

Kitabu hiki kimechaguliwa kuwa ‘Writers Guild Book Club – Book the Month.’ (Mwezi Juni)